Saturday, April 11, 2020

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:FASIHI KWA UJUMLA

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:FASIHI KWA UJUMLA

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:FASIHI KWA UJUMLA

UNAWEZA JIPATIA NOTES ZETU KWA KUCHANGIA KIASI KIDOGO KABISA:PIGA SIMU: 07872327719

ALSO READ;

 1. O’ Level Study Notes All Subjects
 2. A’ Level Study Notes All Subjects
 3. Pats Papers

FASIHI KWA UJUMLA NADHARIA YA FASIHI SANAA

Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifu umbo ambalo msanii hulitumia katika kufikishia ujumbe aliokusudia kwa jamii / hadhira.

AINA ZA SANAA

a)     Sanaa za ghibu (muziki)

Inategemea na matumizi ya ala za muziki (vifaa, sauti) uzuri wa umbo la sanaa ya muziki upo katika kusikia. Sanaa hii hailazimishi fanani (msanii) na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja. Mtunzi hufanya kazi kwa wakati wake na hadhira husikiliza kwa wakati wake.

b)     Sanaa za ufundi

Sanaa hizi hutokana na kazi za mikono. (Mfano: uchoraji, ususi, ufinyanzi, uchongaji, uhunzi, utalizi/udalizi n.k.)

Mfano; – uchoraji hutegemea sana kuwepo kwa kalamu, karatasi, kitambaa, brashi, rangi n.k. uchongaji huhitaji mundu, gogo, tupa, n.k.  Uzuri wa umbo na sanaa za ufundi upo katika kuona. Sanaa hii hailazimishi fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja.

c)     Sanaa za maonesho

Ni kazi mbalimbali za Sanaa ambazo hutegemea utendaji (mfano: ngoma, maigizo, majigambo, matambiko n.k) sanaa zilizomo kwenye kundi la sanaa za maonesho ni lazima ziwe na sifa zifuatazo:-

-Fanani

-Dhana inayotendeka

-Hadhira

-Mandhari

Sanaa za maonesho zinalazimisha fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja, kwani uzuri wa umbo la sanaa hii upo katika kuona utendaji.

a)     Fasihi

Sanaa hii inategemea ufundi wa matumizi ya lugha. Msanii ni lazima awe na uwezo wa kutumia vionjo vyote vya lugha (mfano; methali, misemo, tamathali za semi, nahau, vitendawili n.k)

Fasihi ni sanaa inayotumia lugha kufikisha ujumbe unaokusudiwa kwa hadhira inayokusudiwa. Sanaa hii pia hailazimishi fanani na hadhira kuwa pamoja, mahali pamoja.

KIELELEZO CHA SANAA

     E:\..\..\..\thlb\cr\tz\__i__images__i__\x261.jpg

Kila kipengele cha Sanaa kinatofautiana na kingine kwa umbo na matumizi. Fasihi ni kipengele cha sanaa kinachotumia maneno kuumba huo uzuri wa kisanaa

TOFAUTI KATI YA FASIHI NA TANZU ZINGINE ZA SANAA

        i.            LUGHA

  Kazi zote za fasihi zinaundwa kisanaa kwa kutumia lugha inayotamkika na inayoandikika ambayo hubeba ujumbe fulani tofauti na sanaa zingine kama vile.

–          Ufinyanzi hutumia udongo

–          Uchoraji hutumia kalamu, rangi, karatasi au kipande cha nguo.

     ii.            WAHUSIKA

Kazi ya fasihi hulazimika kuwa na wahusika wake ambao matukio mbalimbali yanayohusu jamii inayowazungukia. Hutumika kutoa dhamira ya mwandishi, Pia hutumiwa kuwasilisha tabia za watu waliomo ndani ya jamii

   iii.            MANDHARI

Fasihi huwa na mandhari ambayo huonyesha tukio linapofanyika. Mandhari inaweza kuwa ya kubuni au ya ukweli.

   iv.            UTENDAJI

Utendaji hujitokeza hasa katika kazi ya fasihi simulizi ambazo hushirikisha hadhira na fanani mahali pamoja na kwa wakati mmoja, Hapa fanani huweza kuonesha matendo katika usimuliaji wake.

      v.            FANI NA MAUDHUI

Fasihi ina sehemu hizi mbili za fani na maudhui ambazo hutegemeana na hufungamana. Fani ni namna msanii anavyosema kuhusu kile kinachosemwa wakati maudhui ni kile kinachosemwa na msanii.

USANAA WA FASIHI

Usanaa wa fasihi hujitokeza katika vipengele vifuatavyo:

 1. Mtindo

Sanaa katika fasihi hujidhihirisha katika namna ya kueleza jambo, Hapa kinachoangaliwa zaidi ni zile mbinu mbalimbali zinazotumiwa na msanii katika kueleza jambo husika. Jambo huweza kuelezwa katika fumbo kwa kupitia; shairi, tamthiliya, hadithi, kitendawili n.k.

 1. Muundo

Huu ni mpangilio mzuri wa visa na matukio. Matukio katika kazi za fasihi hupangwa kiufundi ili yaweze kuwasilishwa vizuri kwa hadhira au jamii husika.

 1. Uteuzi mzuri wa “lugha”:

Iliyojaa vionjo mbalimbali kama vile nahau, misemo, tamathali za semi, taswira na ishara. Lugha inaweza kuchekesha, kukosoa, kukejeli, kubeza, kushawishi n.k

 1. Uundaji mazuri wa “wahusika”.

Wahusika huumbwa kulingana na nia na lengo la mwandishi kwa hadhira wake.

 1. Ujenzi mzuri wa “Mandhari”.

Kazi ya fasihi ni lazima iwe kwenye madhari maalum. Mandhari ikijengwa vizuri husaidia sana kujenga hisia inayokusudiwa na mwandishi kwa hadhira wake ili iwezeshe pia kufiksha ujumbe mahsusi uliokusudiwa.

FASILI ZA FASIHI

FASIHI NI KIOO

Fasihi ni kioo kwa kuwa fasihi inaweza kufananishwa na kioo. Kioo katika maisha ya kawaida huweza kumuonesha binadamu mazuri aliyonayo au mapungufu aliyonayo ili aweze kujikubali au kujikataa. Hivyo fasihi pia ina uwezo wa kuonyesha mazuri au mapungufu yaliyomo ndani ya jamii, aidha kwa jamii au kwa baadhi ya vikundi vilivyomo ndani ya jamii ambavyo huweza kuwa tofauti na mahitaji ya jamii nzima.

Udhaifu:

-Udhaifu unaojitokeza katika fasihi hii ni kwamba fasihi ina uwezo wa kuonesha mambo kama ni mabaya au mazuri lakini haina uwezo wa kuonesha njia ya kutatua matatizo hayo kama kilivyo kioo.

Udhaifu  wa  fasili ya fasihi ni hisi

Je  ni mara ngapi mwanafasihi ataguswa ndipo aweze kuandika kazi ya fasihi?  Je ni mwandishi pekee ndiye anayetakiwa kuguswa?  Ukweli  ni kwamba sio kazi zote zinazoandikwa zinataokana na mguso unaompata mwandishi.

 1.    FASIHI NI MWAMVULI

Fasili ya fasihi ni mwamvuli ilifananishwa na mwamvuli kwa jinsi inavyoweza kumhifadhi binadamu kwa jua au mvua lakini nadharia halisi ya fasili kufananishwa na mwamvuli ni katika uelekeo wa kwamba fasihi inauwezo wa kulinda amali za jamii zisipotee na zisiweze kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.

Udhaifu: – fasili hii ilionesha udhaifu wa fasihi kutokuwa na uwezo wa kulinda amali za jamii yaani mila na desturi zilizopotea kwani mila na desturi ndani ya jamii huwa zinaenda na wakati na hubadilika kulingana na mahitaji ya wakati huo.

iii. FASIHI NI HISI

Dhana hii ilikuwa na maana kwamba kazi ya fasihi inapoletwa mtoaji/ msanii ni lazima awe anaguswa na jambo fulani na ndipo aweze kuandika kazi hiyo.

 1. FASIHI NI KIELELEZO CHA KISANAA

Fasihi inatazamwa Kama ni ubunifu au ufundi wa aina fulani unaojidhihirisha katika maandishi.

Udhaifu: – fasili hii huzingatia zaidi utoaji wa burudani tu na hauzungumzii lolote juu ya uelimshaji wa nini kifanyike juu ya tatizo alilolionesha msanii.

 1.  FASIHI

Fasihi ni sanaa inayotumia lugha ambayo msanii huitumia ili kuweza kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa. Fasihi huwa ina umbo timillifu, Mfano kazi ya fasihi inaweza kuwa tamthiliya (igizo), hadithi au ushairi.

Uhai wa lugha katika kazi ya fasihi inaongeza mvuto. Lugha inaweza kupewa uhai huo kwa kutumia tamathali za semi kama vile tashibiha, tasfida, sitiari, kejeli, dhihaka, balagha kijembe n.k. vipengele vingine vinavyotawala ufasihi ni uundaji wa wahjusika, maatumizi ya picha, mandhari, utendaji, n.k

Mfano:-

Mtoto aloumbika, mara mtoto laini

Shingo yake ya birika, watabasamu moyoni

Kweli asali tamu, wajua ilivyoundwa

Hapa unaweza kupata ujumbe kwa kupitia maswali mbalimbali.

 • Mhusika ameumbwaje?
 • Shingo yake inafananishwa na nini
 • Uzuri wa mototo umeoneshwaje?
 • Asli imetumika kwa sababu gani?
 • Swali lililo kwenye mstari wa mwisho limeulizwa kwa sababu gani?

MADHUMUNI YA FASIHI

Fasihi ni kazi inayotokana na jamii na ipo kwa ajili ya jamii.

Kazi ya fasihi na fasihi yenyewe huathiriwa na mazingira na maendeleo ya jamii.

MADHUMUNI

Fasihi hushughulikia mahusiano ya jamii, hivyo basi fasihi:-

 1. Hueleza ukweli wa maisha ya jamii
 2. Hujenga udadisi kujielewa na kuelewa watu wengine
 3. Huendeleza, hudumisha na kurithisha utamaduni wa jamii
 4. Huonesha jamii njia na mitindo mbalimbali ya kujieleza
 5. Huburudisha kupitia mvuto ulimo ndani ya LUGHA, MUUNDO na MAUDHUI yake.
 6. Huijenga jamii kifikra na kisiasa ili kuwezesha kutoa maamuzi na kuwa na msimamo wa maamuzi hayo.

DHIMA YA FASIHI

1)     Huelimisha, katika kupitia maonyo (huonya) hutohamisha ukweli, huelekeza, hutoa mawaidha na kuonesha mwanga wa migogoro.

2)     Huburudisha  kupitia   maliwazo  (huliwaza),    hufundisha,hubembeleza, huhamasisha, hutuliza mawazo.

DHIMA YA MWANAFASIHI

1)     Huelimisha

Hufanya kazi ya kuelimisha kwa kukosoa, kutia hamasa, kuonya, kueneza mawazo na falsafa za jamii

2)             Huburudisha

3)             Huhifadhi na kurithisha amali za jamii.

4)            Hudumisha na kuendeleza lugha

MATUMIZI YA FASIHI

Matumizi ya fasihi hutegemea sana msimamo na mikabala ya wasimulizi na waandishi. Kwa kawaida mtunzi hujiambatisha na tabaka Lake. Kwa hali hii ndiyo maana:

1)            Mwandishi wa tabaka la watawala kutetea kwa  kusifia tabaka hilo

2)            Mwandishi wa tabaka la wakandamizwaji ataandika maudhui ya kujikomboa yaani kulikomboa tabaka lake.

3)           Anayetokana   na udhamini, utunzi wake hulazimishwa kutetea tabaka lisilo lake ama kwa hofu, kwa malipo au yote kwa pamoja.

UHURU WA MTUNZI WA KAZI ZA KIFASIHI

Ni hali ya mwandishi wa fasihi kuwa huru na wazi kutoa mawazo yake na hisia zake kwa jamii bila ya kupingwa na tabaka lolote.

Au  ni ile hali ya kutunga au kuandika kazi yake bila kushinikizwa na mtu, watu au taasisi fulani yenye nguvu kiuchumi, kisiasa na kitawala. Mtunzi wa  kazi ya fasihi anakuwa na uwezo wake binafsi wa kufanya maamuzi juu ya fani na maudhui ya kazi yake.

NGUZO KUU ZA DHANA YA UHURU WA MTUNZI WA KAZI ZA KIFASIHI

1)     UTASHI

Ni hali ya kuamua kuazimia au kukusudia jambo bila kushurutishwa au kuyumbishwa.Moja ya dhima ya mtunzi ni kuiamsha jamii iweze kutambua unyonyaji, ukandamizaji na uonevu uliomo ndani ya jamii ili iweze kuchukua hatua ya kukomesha hali hizo. Hivyo mtunzi anapotimiza dhima hii anaweza kukabiliana na tabaka kandamizi. Hapo ndipo utashi wa mtunzi unapoweza kumwelekeza kusonga mbele na jukumu lake au kuwa kasuku wa kusifia tabaka tawala au kandamizi kwa kufunika maovu ya tabaka hilo au kujiondoa kabisa kwenye ulingo wa fasihi.

 Mfano Ngugi wa Thiong’o aliwahi kuhukumiwa na serikali ya Kenya alipoandika tamthiliya ya “THIS TIME TOMORROW” kwa kukosoa uovu wa tabaka tawala. Utashi umemfanya mpaka leo aendelee na msimamo wake ule ule.

2)     FALSAFA

Mwandishi anapaswa kuwa na falsafa moja inayoeleweka ambayo huyafanya maandishi yaonekane kama kazi moja yenye mwelekeo maalum. Mwandishi akipoteza uhuru huweza kuyumbishwa kirahisi; Mfano mwandishi anaweza kuandika kuhusu ujamaa, kesho akaandika kuhusu mapenzi, kesho kutwa kuhusu ubepari

Mwandishi asiye huru huwa ni mtumwa wa hali mbalimbali za maisha zinazomfanya ayumbeyumbe huku na kule.

3)     SANAA

Mwandishi anapaswa kuwana weledi wa misingi ya aina ya utunzi wa sanaa anayotaka kuitumia kufikisha ujumbe wake. Mfano:  Akitaka kufikisha ujumbe kwa njia riwaya ni lazima ajue barabara misingi ya uandishi wa riwaya vinginevyo msanii hatokuwa na uhuru wa kisinaa maana hatakuwa na namna yenye nguvu ya kukisema hicho alichonacho.

4)     LUGHA

Msanii ambaye hana weledi wa lugha na misingi ya lugha anayoitumia ni lazima atajikuta amefungwa. Hatakuwa na uhuru wa kusema kile kilichomo nafsini mwake kwa ufasaha na kwa mafanikio.

DHIMA YA UHURU WA MWANDISHI

 1. Mwandishi awe huru kuikosoa jamii au kulikosoa tabaka lolote linalokwenda kinyume na maadili ya jamii
 2. Mwandishi awe na falsafa inayoeleweka na utashi
 3. Kuikomboa jamii kutoka katika fikra mbovu za kugandamizwa, kunyonywa na kuonewa na tabaka tawala.
 4. Uandishi wa kikasuku kupungua
 5. Unaifanya fasihi kuwa chombo cha kuikomboa jamii KIUCHUMI, KISIASA, KIUTAMADUNI, KIJAMII NA KIFIKRA.
 6. Mwandishi anakuwa na uhuru wa kuisukasuka jamii bila matatizo yoyote.

UDHAMINI

Udhamini wa kazi ya fasihi ni kitendo cha mtu au chombo fulani kukubali kufadhili au kugharamia kazi ya mtunzi ili iweze kuchapishwa na hatimaye kusambazwa mahali mbalimbali hadi iwafikie walengwa.

AINA ZA UDHAMINI

 1. UDHAMINI WA KISHAWISHI

Huu ni udhamini ambao mdhamini humshawishi mtunzi wa kazi ya fasihi aidha kwa fedha au masilahi mengine. Hali hii humfanya mtunzi kwa hiari yake kuingia katika udhamini.

 1. UDHAMINI WA NGUVU

Huu ni udhamini ambao hutolewa na vyombo vya dola. Mtunzi huingia katika udhamini huu kwa lazima. Dola hudhamini watunzi ili waweze kuandika kile kilichoagizwa na dola. Hivyo mtunzi huandika na kuingia katika udhamini huu kwa nguvu ya dola kwa kuogopa aidha kazi zake kuzuiwa au kuondolewa kabisa katika ulimwengu fasihi.

 1. UDHAMINI WA MTUNZI MWENYEWE

Huu ni udhamini ambao mtunzi mwenyewe hujisimamia binafsi katika kugharamia gharama zote za uhariri, uchapaji na usambazaji wa kazi zake. Mara nyingi hufanywa na watunzi wenye uwezo

 1. UDHAMINI WA MAKAMPUNI YA UCHAPISHAJI

Yapo makampuni mbalimbali ya uchapishaji ambayo hupokea miswaada kisha wanaithamini, wanaihariri, wanaichapisha na kuisambaza kwa wasomaji. Makampuni haya hutoa fedha kwa ajili ya mambo yote hayo kwa matarajio ya kurudisha pamoja na faida wakati wa mauzo ya kazi inayohusika.

DHIMA YA UDHAMINI WA KAZI YA FASIHI .

(a)  Kuwawezesha watunzi wasiokuwa na uwezo wa kifedha   kuchapisha kazi zao na kuzifikisha kwa hadhira.

(b)  Kuibua vipaji vya watunzi. Kwa kawaida kuna watu wengi wenye vipaji lakini hawavitendei haki kwa vile hawana uwezo wa kuendelea na hatua za mbele kama vile uchapishaji na usambazaji.

(c)  Mdhamini hujitangaza. Udhamini humuwezesha mdhamini kujitangaza ama kibiashara au kupata heshima miongoni mwa jamii.

(d)  Ni njia ya kuleta kipato kwa wadhamini. Kwa mfano kwa makampuni ya uchapishaji.

(e)  Kuwapatia watunzi fedha za haraka kabla na baada ya kazi kuuzwa.

(f)   Kuwainua watunzi chipukizi kwa kuwawezesha kufikisha kazi zao kwa hadhira ili ujumbe uliokusudiwa uwafikie waliokusudiwa.

(g)  Kuwafanya watunzi chipukizi kufahamika.

ATHARI ZA UDHAMINI WA  FASIHI.

Udhamini wa kazi za fasihi una athari mbalimabali, zifuatazo ni baadhi ya athari hizo :-

(a)  Mtunzi  huandika kazi yake kulingana na matakwa ya mdhamini. Kwa mfano iwapo udhamini uliotolewa na kazi zilizo katika lugha ya kiingereza, msanii anayetumia lugha ya Kiswahili kuandika kazi zake hawezi kufaidika na udhamini huo.

(b)  Mtunzi hushindwa kuandika mambo kulingana na mtazamo wake halisi juu ya jamii inayo mzunguka.

Mtunzi hushindwa kukosoa uovu hasa unapokuwa unamhusu mdhamini wa kazi yake.Kwa mfano serikali au tabaka tawala.

(c)  Kukua kwa fasihi pendwa kwa mfano riwaya pendwa na, kudumaa kwa fasihi dhati mfano riwaya dhati. Hali hii inatokana na msukosuko wa kibiashara. Fasihi pendwa inauzwa kirahisi sokoni. kwa kuwa na maudhui yenye msisimko kwa mfano upelelezi, usambazaji, mauaji, mapenzi  n.k.

(d)  Mapana ya kijographia na utafiti  wa  fasihi kabla ya kuandikwa hutegemeana na uwezo wa kifedha wa mdhamini.

(e)  Uhuru wa mwandishi hutoweka.

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:FASIHI KWA UJUMLA
4/ 5
Oleh

No comments: