Saturday, April 11, 2020

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:MAENDELEO YA KISWAHILI

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:MAENDELEO YA KISWAHILI

MAENDELEO YA KISWAHILI

ASILI YA LUGHA YA KISWAHILI

Neno asili lina maana kuwa jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza na tunapozungumzia asili ya lugha ya Kiswahili ina maanisha tunachunguza namna lugha hiyo ilivyoanza.  Wataalamu mbalimbali wa lugha wamefanya uchunguzi juu ya asili ya lugha ya Kiswahili.

Uchunguzi huo umejenga nadharia mbalimbali zinazoelezea chimbuko la lugha ya Kiswahili.

Kwa ujumla historia kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili ina matatizo mengi na ndiyo maana kuna nadharia mbalimbali zinazoelezea juu ya asili ya lugha ya Kiswahili.

Miongoni mwa matatizo yanayoikabili historia ya Kiswahili ni pamoja na:

 1. Hakuna uthibitisho kamili juu ya nadharia zinaelezea asili ya lugha ya Kiswahili na kuenea kwake.
 2.  Uchunguzi wa asili ya Kiswahili ulifanywa na wataalamu wa kizungu ambao waliandika historia ya Kiswahili jinsi walivyoelewa wao baada ya kupata ushahidi kidogo tu.
 3. Wazawa hawakushirikishwa ipasavyo katika uchunguzi wa lugha ya Kiswahili.
 4. Hapakuwa na kumbukumbu za kutosha kwa sababu babu zetu hawakujua kusoma wala kuandika hivyo basi kuna upungufu wa kumbukumbu.

Kutokana na matatizo hayo yanayoikabili historia ya Kiswahili kuna nadharia mbalimbali zinazoelezea historia ya lugha ya Kiswahili.  Nadharia hizo ni kama vile:-

(i) Kiswahili asili yake Kongo

(ii) Kiswahili ni kundi au pijini

(iii) Kiswahili ni lugha ya vizalia

(iv) Kiswahili ni Kiarabu

(v) Kiswahili ni Kibantu.

 1. KISWAHILI ASILI YAKE NI KONGO

Baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili yake ni Kongo (Zaire).  Madai haya yanaimarishwa zaidi na wazo jingine linalodai kwamba katika vipindi lengwa vilivyopata kuwepo sehemu za Pwani ya Afrika Mashariki hazikuwa zimekaliwa na watu. Lakini kutokana na hali ya uzito, ufugaji, na biashara inadaiwa kuwa wabantu walisambaa Afrika Mashariki kupitia Kigoma na baadhi ya sehemu za Uganda.  Wakati wa kusambaa kwao walieneza pia lugha zao kikiwemo Kiswahili.

UDHAIFU

Madai kuwa asili ya Kiswahili ni Kongo hayana msingi kwa sababu mpaka sasa wataalamu wa nadharia hiyo hawajaweza kueleza na kuthibitisha kisayansi ama kihistoria juu ya lini hasa watu walianza kuishi Pwani ya Afrika Mashariki.

II.    KISWAHILI NI KRIOLI AU PIJINI

Baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili ya Kiswahili ni tokeo la mwingilio baina ya wenyeji wa Pwani ya Afrika Mashariki na wageni wa kiarabu. Wataalamu hawa hudai kuwa Kiswahili ni lugha ya kati iliyozuka ili kurahisisha au kufanikisha mawasiliano katika shughuli ya biashara ya mwanzo. Wataalamu hawa husisitiza kuwa lugha ya Kiswahili haikuwepo kabisa kabla ya hapo. Wanaona lugha ya Kiswahili ilianza kama pijini na baadaye kukua na kuwa kama Krioli kutokana na lugha hiyo kuwa lugha ya mwanzo kwa wazungumzaji.

Pijini ni nini?

Ni lugha ambayo huzuka kutokana na kuwepo pamoja kwa makundi mawili yanayotumia lugha mbili tofauti. Ili makundi hayo yaweze kuwasiliana, huundwa lugha ambayo kitabia ni tofauti na zile zinazozungumzwa na makundi yanayohusika.  Lugha hii inaweza kuwa na msamiati kutoka katika lugha moja kati ya hizo mbili, au inaweza ikawa na msamiati wenye uzito sawa.  Lugha hii ndiyo huitwa Pijini.  Pijini huzuka kutokana na vitu kama vile biashara, utumwa, ukoloni, n.k

Krioli ni nini?

Kwa kawaida watu wanaozungumza lugha ya pijini wanaweza kuzoeana na kuishi kwa pamoja hata kuoana. Watoto watakaozaliwa hutumia lugha ya pijini kama lugha yao ya kwanza.  Lugha hii inayotumiwa na watoto hawa watakaozaliwa huitwa krioli.  Krioli ni pijini iliyokomaa.

Wataalamu wa nadharia hii hutumia kigezo cha msamiati uliopo katika lugha ya Kiswahili ambao kwa kiasi kikubwa unatoka katika lugha ya Kiarabu. Ni kweli kuwa lugha hii inamchango mkubwa wa msamiati katika lugha ya Kiswahili.

UDHAIFU

Hutumia kigezo kimoja cha msamiati peke yake kama kigezo pekee ni udhaifu kwa kuwa lugha inaweza kutazamana kwa kutumia vigezo vingine, matamshi, maumbo ya maneno au miundo ya sentensi.  Ukitumia vigezo mbalimbali vya uchambuzi wa lugha, lugha ya Kiswahili ina mfanano zaidi na lugha za kibantu kuliko madai yaliyotolewa na nadharia hii.

III. KISWAHILI NI KIARABU

Kuna madai kwamba lugha ya Kiswahili asili yake ni Kiarabu.  Wataalamu wa nadharia hii hutetea madai yao kwa hoja kuu tatu:-

 1.  Idadi kubwa ya maneno yaliyomo katika Kiswahili takribani 30% ni maneno yenye asili ya Kiarabu. Hivyo basi ni uthibitisho tosha kwamba Kiswahili kilianza kama pijini ya Kiarabu.
 2. Neno lenyewe, Kiswahili; ambalo asili yake ni Kiarabu.  Neno Kiswahili limetokana na neno ‘sahil’ ambalo ni neno la Kiarabu lenye maana ya ‘Pwani’ na neon ‘Swahili’ hutumika likiwa na maana ya ‘Pwani”. Kwa hiyo neno, ‘waswahili’ lina maana ‘watu wa pwani’.
 3. Dini / Biashara / Mila na desturi.  Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianzia Pwani  na kuwa kuna idadi kubwa ya wenyeji wa Pwani ni waislamu kwa imani zao, na kwa kuwa uislamu uliletwa na waarabu, basi hata Kiswahili nacho kililetwa na waarabu.

UDHAIFU

 1. Kutumia kigezo cha msamiati ni udhaifu kwa sababu kila lugha huchukua msamiati kutoka lugha nyingine.  Kiswahili hakikuchukua msamiati kutoka Kiarabu pekee pia lugha nyingine kama: Kiajemi, Kireno, Kihindi, Kijerumani na Kiingereza.
 2. Lugha huchukua msamiati mwingi kutoka lugha fulani si kigezo cha kuhalalisha kuwa lugha fulani ina asili fulani mfano: Kiingereza huchukua maneno kutoka lugha ya Kifaransa, haiwezekani kuhitimisha kuwa Kiingereza ni Kifaransa.
 3. Pia kutumia kigezo cha dini ni udhaifu.  Kwa mfano hatuwezi kusema Kiingereza ni Ukristo kwa kuwa Waingereza ni Wakristo kwa imani yao.  Pia nchi kama Senegal ambayo ina Waislamu wengi lugha ya Kiswahili haizungumzwi huko.  Ni wazi kuwa Uislamu ungekuwa unafungamana na Kiswahili, kingezungumzwa kila sehemu ambapo Uislamu umeenea.

IV. KISWAHILI NI KIBANTU

Nadharia hii hutumia ushahidi wa kiisimu na kihistoria kuchunguza lugha ya Kiswahili katika mfumo mzima wa kihistoria wa mgawanyiko na usambaaji wa lugha za kibantu .  Nadharia hii inaungwa mkono na wataalamu kama Malcom Guthrie, C. Meinhoff na C. Rohl.  Wataalamu hawa huhitimisha kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lugha ya jamii kubwa ya lugha za kibantu.  Nadharia hii ndiyo inaelekea kukubalika- kwa wengi kuwa ndiyo sahihi katika kuelewa asili ya Kiswahili.  Kwa sababu nadharia hii imethibitishwa kwa hoja za kiisimu na hoja za kihistoria.

A. USHAHIDI WA KIISIMU

Ushahidi wa kiisimu ni ushahidi unaothibitishwa kwa misingi ya sayansi ya lugha.  Isimu huchunguza lugha kwa undani kwa kutumia tanzu zake. Baada ya kufanyiwa utafiti wa kina na wataalamu mbalimbali, ilithibitika kuwa asili ya Kiswahili ni kibantu kutokana na vigezo vifuatavyo:-

 • Utafiti wa Malcom Guthrie

Ni mtaalamu wa isimu kutoka chuo kikuu cha London, aliyefanya utafiti wa kutafuta uhusiano kati ya lugha ya Kiswahili na lugha za kibantu kwa miaka 20 katika nchi za Kiafrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinasadikika kuwa ndipo wabantu wanapoishi.

 Katika utafiti wake alichunguza mizizi ya maneno 22,000 kutoka lugha za Kibantu ikiwemo lugha ya Kiswahili

Katika utafiti wake aligundua mambo yafuatayo:-

(a) Mizizi 2,300 ilizagaa katika lugha mbalimbali za kibantu ikiwemo lugha ya Kiswahili.

(b) Mizizi 500 iliungana katika lugha zote 200 alizozifanyia utafiti.

(c) Alipolinganisha lugha hizo na lugha ya Kiswahili, zilionesha ulinganifu kama ifuatavyo:-

– Kiwemba (Zambia) kililingana na Kiswahili kwa 54%.

– Kiluba (Katanga) kililingana na Kiswahili kwa 51%

– Kikongo (DRC) kililingana na Kiswahili kwa 44%

– Kiswahili cha (A. Mashariki) 44%

– Kisukuma (Tanzania) 41%

– Kiyao (Tanzania, Msumbiji) 35%.

– Kirundi (Burundi) 43%

– Kisotha (Botswana) 20%

Mtaalamu huyu pia aligundua kadri unavyoshuka Kaskazini ya Katanga ndiyo msamiati unavyoachana zaidi,

 • Mfanano wa msamiati

Ushahidi huu ulitokana na utafiti wa Prof. Maganga ambaye alibaini kuwa 60% ya maneno ya Kiswahili yenye kuandikika na kutamkika, yana asili ya Kibantu.  30% ya msamiati wa lugha ya Kiswahili unatoka katika Kiarabu na 10% inatoka katika lugha nyingine mfano: Kireno, Kiingereza.

Ni wazi kuwa msamiati wa Kiswahili na Kibantu hautofautiani sana, hasa katika matamshi:-

E:\..\..\..\thlb\cr\tz\__i__images__i__\X1.jpg

 • Miundo  ya tungo:-

Miundo ya tungo za maneno ya Kiswahili inafanana na miundo ya tungo za maneno ya Kibantu.  Mfano:  miundo ya sentensi za Kiswahili huwa na muundo wa Kiima na kuarifu hali kadhalika miundo ya sentensi za Kibantu huwa na muundo huo huo.

Mfano:-

–   Mama / anakunywa maji  (Kiswahili)

        K            A

–   Mayo / aling’wa minze  (Kisukuma)

        K               A

–   Jubha / ikonwa amesi  (Kinyakyusa)

        K                A

–   Yubha / inywa lulenga    (Kihehe)

        K               A

–   Mawe / ang’wa mazi       (Kiha)

       K                  A

NB:  Pia miundo ya sentensi za Kiswahili hubadilika katika maumbo ya umoja na wingi.

Pia maumbo ya kibantu hubadilika katika maumbo ya umoja na wingi.

 

Mfano:  Watoto / wanakunywa maji  (Kiswahili)

–  Mwana / ikonwa amesi   (Kinyakyusa)

            K         A

–   Mwana / avana vinywa lulenga (Kihehe)

      K               A

–  Bhana bhaling’wa minze (Kisukuma)-umoja

            K                     A

–   Bhana / bhaleng’wa minze  (Kisukuma)-wingi

            K                     A

 

 •  Ngeli za majina

Makundi ya majina mbalimbali katika lugha ya Kiswahili huwa na makubaliano kwa kufuata maumbo ya umoja na wingi pamoja na upatanisho wa kisarufi.

Tabia hizi za majina ya Kiswahili hujitokeza pia katika majina ya Kibantu;

(a) Kwa kutumia maumbo ya majina.

Majina mengi ya Kiswahili huwa na maumbo ya umoja na wingi, halikadhalika kwa majina mengi ya Kibantu.

Mfano: Kiswahili               m-toto                         wa-toto

           Kisukuma              ng’-ana                        bh-ana

           Kinyakyusa            mw-ana                       b-ana

           Kihehe                  mw –ana                      v-ana

           Kiswahili                ki –ti                           vi – ti

           Kinyakyusa            ki-goda                        vi-goda

           Kihehe                  ki-kota                         vi-kota

(b) Kigezo cha upatanisho wa kisarufi.

Kwa kutumia kigezo hiki, nomino za Kiswahili na za kibantu hufuata upatanisho wa kisarufi kwa kupachika viambishi pia.  Viambishi hivyo hubadilika kutokana na mabadiliko ya maumbo ya umoja na wingi.

Mfano:     Mtoto mzuri anakunywa maji

                Watoto wazuri wanakunywa maji

                Mwana mnunu ikonwa amesi

                Bana banunu bikonwa amesi

                Mwana mnofu  inywa  lulenga-umoja

                Vana  vanofu vinywa lulenga-wingi

 •  Vitenzi vya Kiswahili na vya Kibantu

Tabia ya vitenzi hivi hufanana.  Mfanano huo hujitokeza katika vipengele vifuatavyo:-

(a)       Viambishi

Lugha ya Kiswahili na kibantu, vitenzi vyake huwa na mzizi pamoja na viambishi awali na tamati.

Mfano:  Kiswahili           a – na – lim – a

            Kindali               a – ku – lim – a

            Kikurya             a – ra – rem – a

1 –  viambishi  vya nafsi

2 – Viambishi vya wakati

3 –  mzizi

4 –  Viambishi tamati maana.

(b) Vitenzi vya lugha ya Kiswahili na Kibantu vina tabia ya kunyumbuka

KiswahiliKuchekakuchekeshaKuchekeleakuchekwa
KinyamweziKusekakusekeshakusekelelaKusekwa
KindaliKusekaKusekeshakusekelelakusekwa
KipogoroKusekakusekesakusekelelaKusekwa
KibenaKuhekakuhekeshakuhekelelakuhekwa

(c)  Mwanzo wa vitenzi

            Vitenzi vya Kiswahili na Kibantu huanza na viambishi vya nafsi mwanzoni.

            Mfano:  Ni – nakwenda

– ni  – sumwike

– ni – ngenda

(d)  Mwisho wa vitenzi

Vitenzi vingi vya lugha ya Kiswahili na vile vya kibantu, huishia na irabu (‘a’) mwishoni.

Mfano:-       

Kukimbia – aKuwind- aKushuk – akiswahili
Kupil-aKuhwim –aKutend – akisukuma
Kukimbil -aKufwin- aKuwik -akihehe

B.  USHAHIDI WA KIHISTORIA

Licha ya ushahidi wa kiisimu, pia kuna ushahidi wa kihistoria unathibitisha kuwa Kiswahili ni Kibantu.

Ushahidi huo unathibitishwa na wageni mbalimbali waliofika Afrika Mashariki na kudhihirisha kuwa Kiswahili kilizungumzwa Pwani ya Afrika Mashariki kabla ya ujio wa wageni.

Ushahidi huu ulitolewa na wageni mbalimbali waliofika Afrika ya Mashariki na kuthibitisha kuwa kabla ya kufika kwao, Kiswahili kilizungumzwa.Wageni hao ni kama wafuatao:-

 • Ushahidi wa Marco Pollo

Ni mwanataaluma wa Kizungu aliyejishughulisha na masuala mbalimbali ya Kijiogragia na kusafiri sehemu nyingine duniani.

 Katika moja ya maandiko yake, anasema hivi; “Zanzibar ni kisiwa kilicho kizuri ambacho kinamzunguko wa maili 200” Watu wake wanaabudu Mungu. Wana mfalme na wanatumia lugha yao na hawalipi ushuru kwa mtu

Nukuu hii imenukuliwa kutoka kitabu cha “SAFARI ZA MARCO POLLO(1958 – 301). [Penguin Books]

Pia katika kitabu chake cha Kijiografia ambacho hakikuchapishwa lakini kimetafsiriwa kwa Kirusi na Kifaransa lakini kina maneno kama vile; Ungudya ambako sasa ni Unguja.  Zanguaba ambako sasa ni Zanzibar.  Maneno mengine ni kama; kundi, firi, Omani, Murijani, na kisuka. Haya ni majina ya aina mbalimbali za ndizi zilizopatikana Zanzibar.

 •  Ushahidi wa Al – Masoud (915 BK)

Katika moja ya maandishi yake anazungumzia juu ya wakazi wa mwambao ambao walijulikana kwa jina la Waenji.  Kwa dhana hii neno Zanzibar linatokana na neno Zanjibar, yaani pwani ya Zanji.

Al – Masoud anaonesha kwamba, Wazanji walikuwa na watawala kwa nguvu za Mungu.  Viongozi hawa walikuwa wacha Mungu, Huenda neno Wakitumia / ina maana ya wafalme.  Anasisitiza kuwa walisema lugha fasaha na walikuwa na viongozi walio hutubia kwa lugha yao.  Kutokana na neno Zanji inawezekana kabla ya kuja kwa waarabu, Kiswahili kilikuwa Kizaramo au Kizanji.

 • Historia ya Kilwa

Kimsingi habari hizi zinaeleza historia ya Kilwa, karne ya 10 mpaka 16 BK na zinahusiana na kutaja majina ya utani kama vile Mkoma watu, Nguo nyingi n.k Ambayo walipewa Masultan wa kwanza wa Kilwa ambao ni Ali Ilbin Hussein na mwanawe.  Mohamed Ibin Ali kutokana na habari hizi huenda lugha ya Kiswahili ilianza kuzungumzwa kuanzia karne ya 10 au 11.

Maelezo ya kihistoria yanaeleza juu ya Sultani aliyeitwa Talt Ibin Al – Hussein aliyepewa jina la utani Hasha haefiki

 • Ushahidi wa Ibin Batuta (14 BK)

Mohamed Bin Abdallah Ibin Batuta ana asili ya kiarabu alifika Afrika Mashariki kunako mwaka 1331 BK, Katika maandishi yake anaeleza maisha ya watu wa nchi ya Afrika Mashariki ingawa yeye aliita nchi ya Waswahili.  Anataja miji kama vile Mogadishu, na Kilwa.  Alisema, “Basi nilianza kusafiri baharini kutoka Mogadisho kwenda nchi ya Waswahili na Kilwa ambao umo katika nchi ya Zanji. Tulifika Mombasa kisiwa kikubwa, mwendo wa siku mbili kutoka nchi ya waswahili, Watu hawajishughulishi na kilimo ingawa huagiza nafaka toka kwa waswahili.”

 •  Maandishi ya Morrice

Maandishi haya yalijitokeza mwaka 1779, Katika maandishi hayo Morrice anawagawa watu wa Afrika Mashariki katika makundi matatu, ambayo ni waarabu, wasuriana na waafrika.  Anasisitiza kuwa masuriana na waafrika walishakaa na kuwa kundi moja.  Wakaelewana na kusema lugha moja ya kisuriana.  Kuna kuwa huenda kisuriana ndicho Kiswahili cha leo.

 • Ugunduzi wa Ali Idris

Ugunduzi huu ulifanywa huko Sicily mwaka 1100 mpaka 1166 BK kwenye mahakana ya mfalme Roger II, Katika ugunduzi huu ilisadikika Kiswahili kiliandikwa kabla ya karne ya 10 BK. Al Idrisi alikuwa wa kwanza kugundua jina la zamani la Zanzibar kuwa ni Ungudya.  Katika maelezo yake anaandika pia majina ya aina za ndizi mbalimbali zilizopatikana huko Ungudya kama vile kikombe, mkono wa tembo, sukari, na muriani.

 • Vitabu vya Periplus na Yu – Yanga Tsa  – Tsu:-

–  Kitabu cha Periplus

Hiki kinahusu mwongozo wa bahari ya Hindi na inasadikika kuwa kiliandikwa karne I katika mji wa Alexander.  Kitabu hiki kinataja habari za Azania yaani Afrika Mashariki na habari za vyombo vya baharini kama vile ngalawa, madema na mitepe.  Kitabu hiki kinaeleza kuwa watu wageni hutozwa ushuru na wafanyabiashara wenyeji na wanaijua pia lugha ya wenyeji vizuri.

–  Kitabu cha Yu- Yanga Tsa  – Tsu

Kitabu hiki kinaeleza habari za upwa wa Afrika Mashariki na shughuli mbalimbali za Wachina hapa Afrika mashariki.

–   Chu – Fan – Chi

Kilichapishwa 1226 na kinaeleza bahari za Zanzibar na shughuli mbalimbali za Wachina hapa Afrika Mashariki.

 •  Ushairi wa Kiswahili.

–  Utenzi wa Fumo Lyongo

Hili ndilo shairi la zamani kabisa.  Lilipata kuandikwa katika lugha ya Kiswahili na inasemekana liliandikwa karne ya 13 BK.  Uwepo wa shairi hili unadhihirisha kuwepo kwa Kiswahili kabla ya hapo.  Huenda kilitumika kabla ya karne ya 10 BK.

LUGHA MAMA (LUGHA YA KWANZA), LUGHA YAPILI NA LUGHA RASMI

Lugha rasmi ni ipi?

Ni lugha inayoteuliwa na serikali ili itumike katika shughuli za kiserikali.  Kiswahili

Tanzania ni lugha ya taifa pia ni lugha rasmi.

Sifa za lugha rasmi:-

(i) Yaweza kuwa lugha sanifu au isiwe sanifu lakini pia yaweza kuwa fasaha au isiwe fasaha.

(ii) Inaweza ikawa lugha ya taifa au isiwe lugha ya taifa.

(iii) Huwa haifuati kabila wala mchanganyiko wa makabila yaliyopo nchini.

(iv) Yaweza kuwa lugha ya kigeni kama vile kiingereza, Kifaransa, Kichina.

(v). Hutegemea utawala uliopo madakarani.

Lugha mama (Lugha ya kwanza):-

Ni lugha ambayo mtu hujifunza utotoni baada tu ya kuzaliwa, kabla ya kujifunza lugha

ya pili.  Mtoto hujifunza lugha hii kwa kusikiliza kutoka kwa wazazi au majirani.  Lugha

hii ni rahisi kujifunza kulingana na ya pili kwa sababu zifuatazo:

(i) Mtoto huwa na muda mrefu wa kujifunza (usio koma)

(ii) Mtoto hujifunza lugha katika mazingira halisi, mfano vile anavyojifunza vipo pale pale.

(iii) Uhusiano wa mtoto na wanaomzunguka kuwa mzuri.

(iv) Kuna kuwa na msaada wa kutosha katika kujifunza.

(v)  Kuna kuwa na uzoefu katika lugha hiyo hiyo moja.

Dhima ya lugha ya kwanza:-

Kukidhi haja ya mawasiliano kwa watu wanaomzunguka mtoto.

NB:   Lugha ya kwanza inaweza kuwa lugha ya pili kwa watu wengine na lugha ya pili

inaweza kuwa ya kwanza kwa watu wengine.  Mfano:  Kiswahili ni lugha ya kwanza kwa

Watanzania wote waliozaliwa mjini lakini yaweza kuwa lugha ya pili kwa Watanzania

waliozaliwa vijijini.

Lugha ya pili:-

Lugha ya pili ni lugha ambayo mwanadamu hujifunza baada ya kujifunza lugha ya

kwanza.  Mara nyingi lugha ya pili huwa na athari ya lugha ya kwanza kuhusishwa na

mazingira ya lugha ya pili.  Kwa Watanzania walio wengi hasa waliozaliwa kijijini

Kiswahili ni lugha yao ya pili.

Matumizi  ya lugha ya pili:-

1. Kutaka kukidhi haja ya mawasiliano kwa jamii ambazo si wazungumzaji wa lugha ya kwanza.

2.  Kutaka kujihusisha na jamii inayozungumza lugha hiyo ya pili.

            Mfano: tunajifunza Kiingereza ili kujihusisha na jamii nyingine.

ii CHIMBUKO LA KISWAHILI

Nadharia hii inazungumzia kuhusu mahali hasa ambapo lugha ya Kiswahili ilichipukia.  Wataalam wa lugha ya Kiswahili wanatofautiana kuelezea mahali hasa ambapo ndiyo chimbuko la lugha ya Kiswahili ilichipukia Kaskazini, Mashariki mwa Kenya na ilitokana na Kingozi na kuna wengine wanadai kuwa Kiswahili chimbuko lake ni Bagamoyo mpaka Mzizima, eneo lililojulikana kama Dar es Salaam hadi Kilwa.  Wataalam hawa wanadai lugha ya Kiswahili ilienea kama Kishomvi.  Madai ya wataalamu hawa hayajawahi kuthibitishwa kwa hoja makini na tafiti zinaonesha kwamba madai hayo hayana ukweli yanahitaji tafiti zaidi.  Kwa ujumla madai haya yanaweza kuwekwa kwenye mchoro kama ifuatavyo:-

     E:\..\..\..\thlb\cr\tz\__i__images__i__\X2.jpg

NB: Kuna kundi la wataalamu wengine linalodai kuwa chimbuko lake ni sehemu mbalimbali za Pwani ya Afrika Mashariki.  Mfano mtaalamu Freeman Grenvill katika makala yake inayoitwa Medieval For Swahili (1959) anadai kuwa lugha ya Kiswahili ilianza na kuinuka katika upeo wote wa Afrika Mashariki kama ambavyo baadhi ya maneno, majina ya watawala na maofisa wa serikali yanavyojitokeza katika fasihi.

Madai ya mtaalamu huyu yanaashiria kwamba watu walioishi katika maeneo mbalimbali ya upande wa Afrika Mashariki walikuwa wakizungumza lugha zao mbalimbali.  Lugha zote hizi zilikuwa za kibantu na hazikutofautiana sana.

 Watu hawa katika kuwasaidia hasa katika biashara walilazimika kurahisisha lugha zao kwa kiasi fulani ili waweze kuwasiliana na miongoni mwao. Urahisishaji huo wa lugha na kuzuka kwa lugha hiyo kubwa ni jambo lililotokea katika sehemu zote za upwa wa Afrika Mashariki.  Matokeo yake kulizuka lugha ambazo zilijulikana kama lahaja za Kiswahili.  Lahaja hizo zilizungumzwa kutoka kusini mwa Somalia hadi Kaskazini-mashariki mwa Msumbiji.

Hapo tunapata lahaja kama vile kitikwa, Kiamu, Chichifundi, Kimvita, Kimombasa, Kimtang’ata, Kimakunduchi, Kihadimu, Kitumbata na Kipemba. Lahaja hizo zinafanana zaidi na lugha mbalimbali za kibantu kuliko zinavyofanana na Kiswahili sanifu kwa kuwa Kiswahili sanifu kina maneno mengi ya mkopo.

 Recommended

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:FASIHI KWA UJUMLA

MASWALI

1. Kwa kutumia hoja madhubuti fafanua chimbuko la lugha ya Kiswahili.

2. Wanadai kuwa Kiswahili ni Kiarabu, wanahoja kubwa kuu tatu.  Fafanua hoja hizo.

3. Kiswahili ni Kiarabu kwa jina lake, lakini ni Kibantu kwa asili yake, thibitisha kwa hoja za kiisimu.

 UFANIFISHAJI WA KISWAHILI
i. Kipindi cha Wajerumani Katika kipindi cha Ukoloni wa Kijerumani, shughuli nyingi za ukuzaji wa Kiswahili kimaandishi zilifanywa na    Wamisionari wa mashirika mbalimbali ya dini. Sera za mashirika hayo ya dini zilielekeza kuwa uenezi wa mafundisho, ya dini            yafanywe kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Kazi kubwa iliyofanywa na mashirika ya dini ilikuwa ni kufundisha lugha ya Kiswahili          shuleni na pia kuhimiza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kutolea mafundisho ya dini.

     Utawala wa Kijerumani kwa wakati huo haukujishughulisha na kukikuza Kiswahili katika eneo la maandishi. Wajerumani walizingatia zaidi kukijua na kukitumia Kiswahili katika shughuli utawala. Hivyo, ilibidi kila akida, jumbe na liwali afahamu Kiswahili barabara ili aweze kutumiwa na utawala wa Kijerumani katika kufanya kazi mahali popote nchini Tanganyika wakati huo. Katika utawala wa Kijerumani, Kiswahili kilikuwa chombo cha kushughuliikia mawasiliano kati ya watawala na watawaliwa hata hivyo, utawala wa Kijerumani ulisaidia kukikuza na kukieneza Kiswahili kwa sababu Wajerumani ulisaidia kukikuza na kukieneza Kiswahili kwa sababu Wajerumani walisisitiza kwamba kila mtu aliye husiana nao moja kwa moja ilibidi atumie lugha ya Kiswahili kwa ajili ya mawasiliano.

ii. Kipindi cha waingereza Mwaka 1879 Askofu Edward Steere ambaye alikuwa Mwingereza wa Shirika la University Mission to Central     Africa( U.M.C.A) aliandika toleo la kwanza la sarufi ya Kiswahili kilichozungumzwa Zanzibar. Kitabu hicho kiliitwa A Handbook of         the Swahili language as spoken at Zanzibar. Sarufi hii imeendelea kutumiwa hadi karne ya ishirini. Pia, shirika la U.M.C.A lilieleza       kutoa vitabu vingi vya dini kama vile sala na nyimbo ambavyo viliandikwa kwa Kiswahili. Vile vile, Shirika la U.M.C.A chini ya A.         Madan ambaye alikuwa bingwa wa lugha lilifanikiwa kutayarisha na kuchapisha kamusi ya Kiswahili –kiingereza na kiingereza-           Kiswahili pamoja na kuandika vitabu mbalimbali vya mafundisho ya dini ya Kikristo kwa lugha ya Kiswahili.

Usanifishaji wa Kiswahili Waingereza ndio waliochukua hatua ya kusanifisha lugha ya Kiswahili mara tu baada ya Tanzania Bara ( Tanganyika) kuwa chini ya utawala wa Waingereza. Juhudi zilifanywa ili kuteua lugha moja ya kienyeji itakayotumika katika elimu ya msingi kwenye nchi zote za Afrika Mashariki yaani Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar. Hatua ya kwanza ya kuelekea usanifashaji wa Kiswahili ilifanyika mwaka 1925 mjini Dar es salaam wakati Gavana wa Tanganyika alipoitisha mkutano wa wakuu wa elimu wa nchi zote za Afrika Mashariki ili kuzungumzia suala la lugha moja ya kufundishia elimu ya msingi.

Hata hivyo mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe kutoka Tanganyika na Zanzibar. Nchi za Kenya na Uganda hazikutuma wajumbe wake ingawa zilikuwa zimealikwa. Wajumbe wote waliohudhuria walipendekeza lugha ya kibantu itumike katika shule hizo. Kiswahili kilipendekezwa lugha ya kibantu itumike katika shule hizo. Kiswahili kilipendekezwa na kuchaguliwa kuwa lugha ya kufundishia. Hata hivyo, Kiswahili wakati huo kilikuwa na mkusanyiko wa lahaja nyingi. Kwa hiyo washiriki wa mkutano wa 1925 waliteua lahaja tatu kutoka miongoni mwa lahaja mbalimbali za Kiswahili ili zipigiwe kura na kupata lahaja moja. Hatua ya pili ya usanifishaji wa lugha ya Kiswahili ilichukuliwa pale mkutano mwingine wa nchi za Afrika Mashariki ulipoitishwa Juni, 5 , 1928 mjini Mombasa.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe wote kutoka Tanganyika, Kenya , Uganda na Zanzibar pamoja na mwanaisimu mashuhuri Carl Meinhof kutoka Chuo cha International Institute of African Language and Cultures. Kati ya mambo muhimu yaliyozungumzwa ilikuwa ni ripoti ya mkutano wa 1925. Katika hauta ya kwanza ya kuteua lahaja za Kiswahili kuliltokea lahaja kuu tatu za kugombania nafasi ya kuteuliwa ili lahaja moja iwe ya kusanifia lahaja ya Kiswahili sanifu. Lahaja zilizoteuliwa ni kimvita, kiamu na kiunguja. Baada ya mvutano mkubwa katika kikao cha halmashauri hiyo yenye wajumbe kutoka nchi zote nne kiamu kiliangushwa na kubakia kimvita na kiunguja. Baadae kiunguja kikashinda katika mjadala mrefu na kimvita kikaangushwa. Maafikiano ya ripoti hiyo yalikubaliwa na nchi zote baada ya marekebisho ya ripoti hiyo yalikubaliwa na nchi zote baada ya marekebisho Fulani kufanywa. Kiunguja kiliteuliwa rasmi kuwa lahaja ya kusanifishia Kiswahili, lahaja ambayo ilipendekezwa awali na Tanganyika katika mkutano wa 1925.
Kiunguja kiliteuliwa kwa sababu kilikuwa kimekwisha enea katika sehemu kubwa na kilionekeana kuwa na uhusiano mkubwa na lahaja nyingine za Kiswahili. Kiunguja kuteuliwa kuwa lahaja ya kusanifiwa lugha ya Kiswahili kutokana na sababu kuu nne kama ifuatavyo;
Kwanza, kiunguja kilikuwa kimekwisha enea sehemu kubwa sana na kueleweka katika nchi zilizokusudiwa yaani Zanzibar, Tanganyika, Kenya na Uganda.
Pili, lahaja ya kiunguja ilikuwa imekwisha tumika katika medani ya kitaaluma na kidini hasa Tanganyika tangu wakati wa wajerumani na sehemu kubwa kuenezwa na wahubiri wa dini ya kiislamu na kikristo.
Tatu, kimvita kilionekana kuwa kigumu kwa wageni wa lugha hii au watumiaji wa Kiswahili ikiwa lugha ya pili ingewapa taabu katika matamshi hasa kwa yale maneno yanayohitajika kutamkwa kwa ncha ya ulimi. Kwa mfano, neno njoo litamkwe “ndoo” na macho yatamkwe “mato” na mengine kadhaa. Kwa hiyo kiunguja kilishinda kwa sababu kilikuwa lugha nyepesi zaidi, kilichoenea sehemu kubwa sana, kimetajirika zaidi kimsamiati na kwa hiyo kilikidhi haja ya watumiaji wa jamii kubwa iliyokusudiwa.

  Na nne, tabaka tawala yaani wakoloni wa kiingereza walipenda kiunguja iwe lahaja ya kusanifishwa Kishili na wao ndio walilopendekeza tangu awali kwenye kikao cha mwaka 1925. Pia katika kikao cha mwaka 1928, waingereza waliendelea na msimamo wao wa kutetea kiunguja iwe lahaja ya kusanifia Kiswahili.

Hatua ya tatu ya muhimu katika usanifishaji wa Kiswahili ilichukuliwa Januari 1, 1930 ambapo kamati iliyoundwa ilianza kazi zake rasmi. Kamati hiyo ilijulikana kwa jina la The Inter-Territorial language (Swahili) committee yaani kamati ya lugha ya Kiswahili za nchi za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa, kamati hiyo ilisimamia shughuli zote za kusanifisha lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:
• Kusanifisha otografia itakayotumika kwa wote kwa kupata maafikiano kamili shughuli zote yaani Tanganyika, kenya, Uganda na          Zanzibar
• Kudumisha ulinganifu wa sarufi kwa kuchapisha vitabu vya sarufi vilivyoafikiwa kwa pamoja
• Kuwatia moyo na kuwasadia waandishi ambao ni wenyeji wa lugha ya Kiswahili
• Kuwapa wale wote waliopo na ari ya kuwa waandishi ushauri juu ya uandishi wa vitabu wanavyokusudia kuandika.
• Kusahihisha lugha ya vitabu vya shule na vinginevyo ambavyo vimekwisha chapishwa mara masahihisho yanayohitajika
• Kutafsiri katika Kiswahili vitabu vya kingereza vilivyochaguliwa kutumiwa shuleni kama vitabu vya kiada na ziada
• Kuchunguza na pale inapokuwa lazima kusahihisha lugha ya vitabu vya ziada kabla ya havijachapishwa
• Kusoma na kuhakiki vitabu vya Kiswahili vilivyoteuliwa na kamati
• kuwapa waandishi wa vitabu maelezo ya taratibu za kufundishia za wakati uliopo katika Nyanja mbalimbali.
• Kujibu maswali yote kuhusu lugha ya Kiswahili na fasihi yake. Mbali na majukumu yaliyotajwa hapo juu, kamati ilitoa maazimio       kadhaa. Baadhi ya maazimio hayo yalikuwa:-
• Kuanzia mwaka 1932, kiunguja kitumike katika shughuli zote za elimu ya chini na
serikalini. Lahaja zitakazokubalika ni zile tu za kiunguja kilichosanifiwa
• Lahaja ya Zanzibar ( kiunguja ) pamoja na marekebisho yote
yatakayofanyikaikubalike kkuwa lugha sanifu.
• Maneno ya kibantu yatatumika kila inapohitajika, pia maneno ya kiarabu na ya lugha
nyingine yaliyojikuta katika matumizi yasipiuuzwe.
• Kitabu cha steere cha Swahili Exercises ma sehemu ya sarufi kiitwacho
Handbook pamoja na kamusi ya madan vikubalike kuwa Kiswahili sanifu.

1. Kiswahili kuwa lugha ya taifa nchini Tanzania Baada ya kupata uhuru hapa Tanzania bara, Kiswahili kilipandishwa hadhi na                 kuteuliwa kuwa lugha ya taifa. Mnamo septemba 1962 Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu J.K.             Nyerere alihutubia Bunge kwa mara ya kwanza kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

2. Kiswahili kutumika kufundishia Elimu Kama tulivyoona hapo juu, baada ya Kiswahili kuteuliwa na kuwa lugha ya Taifa,mwaka 1966     kiswahili kilifanywa kuwa lugha rasmi ya kufundishia katika shule za msingi pamoja na vyuo vya ualimu daraja la tatu “A” Tangu       uhuru hadi sasa pia, Kiswahili ni somo mojawapo la kitaaluma katika shule za sekondari, taasisi mbalimbali na katika vyuo vikuu       ndani ya nchi na hata nchi za nje. Mnano mwaka 1970, serikali ilianzisha idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa     madhumuni ya kutayarisha walimu wenye shahada katika somo la Kiswahili ili waweze kufundisha Kiswahili katika shule za               sekondari na vyo vya elimu nchini Tanzania.

1. Kiswahili kutumika katika kampeni mbalimbali za kitaifa

Kampeni za kitaifa ni harakati za kufanya mambo haraka kwa watu wengi ili umma ufaidike. Mara baada ya uhuru hasa katika kipindi cha Azimio la Arusha, Tanzania iliendesha kampeni mbalimbali za kitaifa kama vile; kupanga ni kuchagua 1969, uchaguzi ni wako 1970, wakati wa furaha 1971, mtu ni afya 1973, chakula ni uhai 1975 nakadhalika. Kampeni zote za kitaifa ziliendeshwa na zilienezwa kwa lugha ya Kiswahili na watu wengi waliweza kujifunza msamiati mbalimbali juu ya uchumi, siasa, elimu, afya, uchaguzi nakadhalika.

2. Vyombo vya habari

Kama tulivyoona katika juhudi za kukuza na kukieneza Kiswahili nchini Tanzania kabla ya uhuru, vyombo vya habari ni mojawapo ya mambo yaliyochangia kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Tanzania. Matangazo kwa njia ya redio yalianza baada ya mwaka 1950 hapa Tanzania bara, kwanza kama sautiya Dar es salaam, halafu baadaye kama sauti ya Tanganyika. Pia katika enzi za kabla ya uhuru hapa Tanzania bara magazeti ya Kiswahili yaliyokuwa yakitolewa kusomwa na wananchi ni kama vile: Mambo leo, habari za leo, tazama, baraza, rafiki yetu na kiongozi.

3. Sherehe na mihadhara mbalimbali ya kiutawala, kijamii, kisiasa na kidini

Harakati za kiutawala na mambo ya kisiasa tangu uhuru hadi sasa huendeshwa katika lugha ya kiswahili. Kwa mfano, Kiswahili hutumika bungeni, mahakamani na kwenye mikutano ya kampeni ya kisiasa hususani kwenye kipindi cha uchaguzi. Pia, shughuli za sheherehe mbalimbali za vyama ambapo wageni rasmi au viongozi wakuu hutoa hotuba zao kwa kutumia lugha ya kisahili. Jambo hili limetoa na linaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiswahili.

4. Kuundwa kwa taasisi (vyombo) mbalimbali za kukuza, kuimarisha na kuendeleza lugha ya Kiswahili Nchini Tanzania tangu uhuru hadi sasa

Kama tuliyvoona hapo juu, baada ya lugha ya Kiswahili kupata hadhi ya kutambuliwa na kuwa lugha ya Taifa, taasisi, mashirka na vyama mbalimbali viliundwa kwa makusudi ya kuendeleza, kukuza na kueneza Kiswahili nchini Tanzania. Baadhi ya vyombo hivyo ni hivi vifuatavyo

 1. Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili (TUKI)

Mwaka 1970, profesa George Mhina aliyekuwa Mkurugenzi wa kwanza mzawa wa TUKI aliyetaja madhumuni ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili kuwa ni

 • Kushughulika na ukuzaji wa maneno ya Kiswahili na utengenezaji wa kamusi ya Kiswahili/ mnamo mwaka 1981 TUKI ilichapisha kamusi ya Kiswahili- Kiswahili. Na mwaka 2004 TUKI ilitoa toleo la pili la kamusi ya Kiswahili ya Kiswahili- Kiswahili.
 • Kuendesha uchunguzi wa lugha kwa madhumuni ya kukukza na kustawisha Kiswahili
 • Kuhifadhi ufasaha wa lugha ya Kiswahili
 • Kuwatia moyo watu wanaojishughulisha na uandishi wa vitabukatika lugha ya Kiswahili
 • Kutafsiri maandishi yafaayo katika Kiswahili
 • Uhariri wa vitabu na utoaji wa jarida la Kiswahili na jarida dogo liitwalo mulika.

Ili kutekeleza majukumu hayo hapo juu, TUKI ilikuwa na sehemu kuu nne ambazo ni fasihi, isimu, uchapishaji na kamusi.

 • Sehemu ya fasihi ilijishughulisha na uchunguzi wa fasihi simulizi na fasihi andishi
 • Sehemu ya Isimu ilijishughulisha na utafiti katika sarufi na matumizi ya Kiswahili pamoja na utafiti wa lahaja mbalimbali Kiswahili.
 • Sehemu ya istilahi na tafsiri ambayo ilishugulikia fani mbili yaani istilahi na tafsiri
 • sehemu ya Kamusi ilishughulikia uundaji wa kamuzi mbalimbali pamoja na kuandaa istilahi ya masomo mbalimbali

NB. Kuanzia mwaka 2009 TUKI imebadili jina na kuitwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahil (TATAKI)

Majukumu

Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ni taasisi ya utafiti na ufundishaji iliyopewa jukumu la kutafiti na kufundisha nyanya zote za lugha ya Kiswahili, fasihi na utamaduni, na uchapishaji wa matokeo ya utafiti huo. TATAKI vile vile ina jukumu la kutekeleza mipango ya sasa nay a muda mrefu ya muda mrefu ya elimuna maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

            Malengo

Malengo makuu ya Taasisi ya taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam ni haya yafuatayo;-

(i) Kufanya utafiti katika Nyanja mbalimbali za mofolojia ya Kiswahili, sintaksia, fonolojia, ismujamii na lahaja

(ii)kufanya utafiti katika leksikografia ya Kiswahili na kutunga kamuzi za jumla na za masomo

(iii)kufanya utafiti na kutunga istilah mpya kwa ajili ya taaluma mbalimbali na /au kwa ajili ya maeneo maalum ya kitaaluma

(iv)kuratibu na kutoa huduma za tafsiri kwa ajili ya ofisi za Serikali, mashirika ya umma, viwanda, taasisi na watu binafsi ndani na nje ya nchi.

(v)Kufanya utafiti wa fasihhi simulizi na fasihi andishi, sanaa za maonyesho, mila na destruri na utamaduni wa mtanzania na wa jamii za Afrika Mashariki

(vi)Kushirikiana na asasi nyingine katika kuendeleza lugha ya Kiswahili na kutoa huduma za ushauri katika Nyanja mbalimbali za lugha ya Kiswahili na fasihi

(vii)Kuchapisha maandiko ya kufundishia Kiswahili katika shule na vyuo

(viii)Kuhakikisha kuwa Kiswahili kinakuwa na msingi mzuri kuwa lugha ya kufundishia katika shule na katika ngazi ya elimu ya juu.

(ix) Kuendeleza Kiswahili kwa kutumia teknolojia mpya.

(ii) Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA)

Chama hiki kilianza kabla ya uhuru tarehe 29/3/1959, lakini kazi zake zilijitokeza rasmi hasa baada ya uhuru. Madhumuni ya chama cha UKUTA yalikuwa:

 • Kuhifadhi na kustawisha lugha ya Kiswahili fasaha na ushairi wake kwa misingi ya kibantu pamoja na kustawisha ushairi ukiwa stadi maalum inayosaidia elimu ya Kiswahili kwa faida ya Taifa zima
 • Kamsha na kkuchochea ari za watu wanaotaka kuwa watalamu katika fani za ushairi
 • Kustawisha utamaduni wa michezo ya ngojera na kuigiza
 • Kuamsha juhudi za wale wanotaka kutunga vitabu vya elimu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili na vya ushairi

Katika uhai wake, chama cha UKUTA kilijishughulisha zaidi uendeshaji wa sanaa za ushairi na ngonjera na kutoa vitabu kadhaa vilivyoitwa Ngojera za ukuta

(iii) baraza la Kiswahili Tanzania ( BAKITA)

BAKITA iliundwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge ya mwaka 1967 ili kutoa mwongozo wa lugha ya Kiswahili nchini. Wanachama wake hutoka katiak Wizara mbalimbali za Serikali, mashirkka na watu binafsi. Kazi za BAKITA NI:

 • Kushirikiana na vyama na vyuo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinavyohusika na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili na kuunganisha juhudi na kazi zao
 • Kutilia nguvu mafanikio ya peo za juu katika kkutumia lugha ya Kiswahili na kuzuia kadri iwezekanavyo matumizi yake mabaya
 • Kukuza maendeleo na matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 • Kushirikiana na Wizara/idara zinazohusika katika kuunda au kutoa tafsiri za maneno ya Kiswahili
 • kutoa jarida la Kiswahili linaloongoza matumizi sahihi ya maneno na maendeleo yake.

BAKITA ina kamati ya kusanifu lugha ambayo iliweka utaratibu ulianza kutumika mwaka 1974 baada ya agizo la Waziri Mkuu wa wakati huo. Utaratibu huo umekuwa ukifanyiwa marekebisho ili kwenda na wakati.

Utaratibu huo unazingatia yafuatayo:-

 • Istilahi mpya zinatakiwa zipatikane kutokana na Kiswahili chenyewe pamoja na lahaja zake
 • Kama istilahi hizi haziwezi kupatikana kuktoka katika Kiswahili, juhudi zinafanywa na kuzitafuta istilahi hizi kutoka katika lugha za makabila ya kibantu
 • Vile vile lugha za makabila yetu ambayo si ya kibantu hufanyiwa uchunguzi ili kuzipata istilahi mpya
 • Neno jipya linaundwa kwa kuunganisha silabi chache kutoka katika maelezo ya neno hilo
 • Maneno mawili au matatu huunganishwa na kupaa neno moja na misingi ya lugha ya Kiswahili

Vile vile, Baraza la Kiswahili Tanzania hutayarisha mijadala redioni kuhusu matumizi bora ya maneno, na wakati mwingine hushughulika na uchunguzi katika matumizi ya lugha ya Kiswahili

(iv) idara ya Kiswahili- Chuo kikuu cha Dar es salaam

Idara ya Kiswahili ilianza mwaka 1970 baada ya/chuo Kikuu cha Dar es salaam kuzaliwa rasmi. Lugha itumiwayo kufundishia masomo ya fasihi, matumizi, miundo na nadharia za isimu ni Kiswahili madhumuni ya idara yalikuwa ni kawaandaa wataalamu wenye shahada katika masomo ya Kiswahili ili waweze kutumia katika Nyanja mbalimbali za maendeleo nchini. Masomo ambayo yamekuwa yakitolewa na idara hii ni fasihi, matumiz, miundo na nadharia za Isimu. Masomo yote haya hufundishwa katika lugha ya Kiswahili tangu idara ya kishwahili ianzishwe, imetoa wahitimu wengi ambao wanafundisha somo la Kiswahili katika shule za Sekondari na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu, pia idara imetoa wahitimu wa shahada ya pili (uzamili) (M.A) na shahada ya tatu ( uzamivu ) (Ph.D)

(v) taasisi ya Kiswahili na lugha za kigeni Zanzibar (TAKILUKI)

Taasisi hii ilianzishwa kwa mujibu wa sheria Na.04 ya mwaka 1979 na kupewa hadhi kuwa shirika. Taasisi ya Kiswahili na lugha za kigeni ( TAKILUKI) inafanya kazi chini ya udhamini wa Wizara ya Elimu- Zanzibar. Baadhi ya kazi za TAKILUKI ni;

 • Kutoa mafunzo na masomo ya Kiswahili kwa kiwango cha juu kwa watumishi wa Serikali kwa ujumla na kuwaingiza katia kunga za Kiswahili fasaha
 • Kuendesha mafunzo ya masomo ya Kiswahili na lugha za kigeni kwa wanafunzi wenyeji na wageni kutoka nje ya Tanzania.
 • Wanafunzi kigeni hupewa mafunzo ya lugha ya Kiswahili katika ngazi ya msingi kati na juu
 • Kufanya utafiti wa lahaja, fashihi simulizi na fasihi andishi ya kiswahili

MADA ZOTE ZA KISWAHILI KIDATO CHA TANO BOFYA HAPO CHINI KWA KILA KUSOMA MAADA

FASIHI KWA UJUMLA 

MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI

MAENDELEO YA KISWAHILI

MATUMIZI YA SARUFI

UTUNGAJI

UTUMIZI WA LUGHA

 

ALSO READ

O, LEVEL FULL STUDY NOTES FOR ALL SUBJECTS

A’ LEVEL FULL STUDY NOTES FOR ALL SUBJECTS

 

 

KISWAHILI KIDATO CHA TANO:MAENDELEO YA KISWAHILI
4/ 5
Oleh

No comments: